Ivory Coast yatangaza kuondoka kwa wanajeshi wa Ufaransa katika taifa hilo la Afrika Magharibi
Ivory Coast imetangaza kuwa wanajeshi wa Ufaransa wataondoka katika taifa hilo la Afrika Magharibi, na hivyo kupunguza zaidi ushawishi wa kijeshi wa mkoloni huyo wa zamani katika eneo hilo.
Katika hotuba ya mwisho wa mwaka, Rais wa Ivory Coast, Alassane Ouattara, alisema hatua hiyo ni kielelezo cha jeshi la kisasa la nchi hiyo.
Nchi jirani ya Senegal, ambayo mwezi uliopita ilitangaza Ufaransa italazimika kufunga kambi zake za kijeshi kwenye eneo lake, ilithibitisha kuwa hatua hiyo itakamilika mwishoni mwa 2025.
Ivory Coast ina kikosi kikubwa zaidi kilichosalia cha wanajeshi wa Ufaransa katika Afrika Magharibi.
Kuna wanajeshi 600 wa Ufaransa nchini humo na 350 nchini Senegal.
"Tumeamua kwa njia ya pamoja kuondoa vikosi vya Ufaransa kutoka Ivory Coast," Rais Ouattara alisema.
Aliongeza kuwa kikosi cha wanajeshi cha Port Bouét ambacho kinaendeshwa na jeshi la Ufaransa kitakabidhiwa kwa wanajeshi wa Ivory Coast.
Ufaransa, ambayo utawala wake wa kikoloni huko Afrika Magharibi ulimalizika miaka ya 1960, tayari imewaondoa wanajeshi wake kutoka Mali, Burkina Faso na Niger kufuatia mapinduzi ya kijeshi katika nchi hizo na kuongezeka hisia za chuki dhidi ya Ufaransa.
Serikali ya Chad ambayo ni mshirika mkuu wa Magharibi katika mapambano dhidi ya wanamgambo wa Kiislamu katika eneo hilo, ilimaliza ghafla mkataba wake wa ushirikiano wa ulinzi na Ufaransa mwezi Novemba.
Rais wa Senegal Bassirou Dioumaye Faye alisema: "Nimemuagiza waziri wa jeshi kupendekeza funzo jipya la ushirikiano katika ulinzi na usalama, linalohusisha, miongoni mwa matokeo mengine, kumalizika kwa uwepo wa jeshi la kigeni nchini Senegal kuanzia 2025."
Faye alichaguliwa mwezi Machi kwa ahadi ya kutoa mamlaka na kukomesha utegemezi kwa nchi za kigeni.
Ufaransa itabaki na uwepo mdogo nchini Gabon.
Viongozi wa kijeshi wa Niger, Mali na Burkina Faso wamesogea karibu na Urusi tangu kuwatimua wanajeshi wa Ufaransa katika nchi zao.
Kisha Urusi ilituma mamluki katika eneo la Sahel ili kuwasaidia kupambana na waasi wa kijihadi.
Kuna dalili kwamba Ufaransa sasa imebaki na wanajeshi wasiozidi 2,000 nchini Djibouti na Gabon.
Wachunguzi wa masuala ya kisiasa wanaamini kuwa Ufaransa imekuwa ikifanya juhudi za kufufua ushawishi wake wa kisiasa na kijeshi unaopungua barani Afrika.
Mamlaka ya zamani ya kisiasa sasa inaonekana kubuni mkakati mpya wa kijeshi wa kupunguza uhusiano wa kijeshi, hatua ambayo ingepunguza kwa kasi uwepo wake wa kudumu wa askari katika bara.
Kwa zaidi ya miongo mitatu baada ya uhuru wake kutoka kwa Ufaransa, Ivory Coast (pia inajulikana kwa jina lake la Kifaransa, Côte d'Ivoire) ilijulikana kwa maelewano yake ya kidini na kikabila, pamoja na uchumi wake uliostawi.
Nchi hiyo ya Afrika Magharibi ilisifiwa kama kielelezo cha utulivu. Lakini uasi wa silaha mwaka 2002 uligawanya taifa hilo sehemu mbili. Makubaliano ya amani yalibadilishwa na ghasia zilizozuka upya huku nchi hiyo ikielekea katika utatuzi wa kisiasa wa mzozo huo.
Licha ya kukosekana kwa utulivu, Ivory Coast ndiyo muuzaji mkubwa zaidi wa kakao duniani, na raia wake wanafurahia kiwango cha juu cha mapato ikilinganishwa na nchi nyingine katika eneo hilo.