Mfungwa wa Guantanamo Bay apelekwa Tunisia
Mwanaume mmoja aliyeshikiliwa katika gereza la Marekani la Guantanamo Bay, Ridah Bin Saleh al-Yazidi amerejeshwa Tunisia, imesema Idara ya Ulinzi ya Marekani.
Pentagon haikusema ikiwa Bw Yazidi alikubali hatia yoyote.
Tangu 2002, kizuizi cha Guantanamo Bay kimetumika kuwashikilia wale ambao Marekani inawataja kama wapiganaji hatari waliokamatwa wakati wa "vita dhidi ya ugaidi.”
Kambi hiyo ni sehemu ya kambi ya jeshi la wanamaji la Marekani kusini-mashariki mwa Cuba.
Kulingana na ripoti ambayo haijathibitishwa na New York Times, Yazidi hakuwahi kushtakiwa na aliidhinishwa kuhamishwa zaidi ya miaka kumi iliyopita.
Gazeti hilo pia lilisema alikuwa Guantanamo Bay tangu kituo hicho kilipoanzishwa mwaka 2002.
Kulingana na taarifa ya Pentagon ya Jumatatu, watu 26 wanashikiliwa Guantanamo Bay, kati yao 14 wanastahili uhamisho.
Mapema mwezi Disemba, Pentagon ilitangaza kwamba Marekani imewarejesha nyumbani wafungwa wengine watatu, shirika la habari la Associated Press liliripoti.
Kambi hiyo ilianzishwa na utawala wa Bush ili kuwaweka kizuizini washukiwa hatari kwa mahojiano na kufunguliwa mashitaka ya uhalifu wa kivita.
Utata umeibuka tangu kipindi hicho kwani washukiwa wameshikiliwa bila kufunguliwa mashtaka na matumizi ya mbinu za mateso za kuwahoji.