"Msimu wa Pili wa Vurugu" dhidi ya Wahamiaji huko Marekani

 

Donald Trump anatazamiwa kuanza rasmi kuhudumu katika wadhifa wa urais wa Marekani tarehe 20 Januari, na anatarajia kuchukua hatua kubwa za kukatisha kasi ya uhamiaji na kuwafurusha wahamiaji haramu kutoka nchini humo.

Mapendekezo ya Trump ya kutekeleza sera za uhamiaji, ikiwa ni pamoja na kumteua Tom Homan kama "Mratibu Mkuu wa Mipaka", yameongeza wasiwasi kwa wahamiaji na baadhi ya maafisa wa Marekani.

Katika muktadha huu, Julian Castro, waziri wa zamani wa makazi Marekani, aliashiria kuwa uteuzi wa Tom Homan kudhibiti mipaka ya Marekani ni mwanzo wa "Msimu wa Pili wa Vurugu" dhidi ya wahamiaji.

Castro alisema: Uteuzi huu unadhihirisha tena "moyo wa vurugu" na kwa maneno mengine, moyo wa uovu wa Homan na timu ya Trump dhidi ya wahamiaji. Wanataka kuwadhalilisha wahamiaji.

Donald Trump tangu mwanzo wa kampeni zake za uchaguzi, daima amekuwa akitangaza azma ya kufukuza wahamiaji haramu na kufunga mipaka ya Marekani kwa wahamiaji wapya hasa kutoka Mexico kama moja ya mipango yake muhimu. Mwezi uliopita, viongozi walichagua watu kama chaguzi za kuyaendeleza sera ya kufukuza wahamiaji wasio halali.

Katika muktadha huu, Rodney Scott aliyekuwa mkuu wa Idara ya Doria ya Mipaka ameteuliwa kuwa kaimu wa Ofisi ya Forodha na Ulinzi wa Mipaka na Caleb Watlow, mfanyakazi wa muda mrefu wa Ofisi ya Wahamiaji na Nidhamu ya Forodha (ICE) ya Marekani, ameteuliwa kuwa mkurugenzi wa ofisi hii; watu ambao watakuwa na jukumu muhimu katika kutekeleza sera za uhamiaji za Donald Trump, ikiwemo ahadi yake ya kufukuza mamilioni ya wahamiaji wasio halali.

Uteuzi wa watu hawa unatokea katika hali ambayo wana historia ya kutekeleza sera za dhuluma dhidi ya wahamiaji, bila kuzingatia haki za kibinadamu za wahamiaji wengi. Kwa mfano, Homan ambaye hapo awali alifanya kazi kama kiongozi wa Idara ya Uhamiaji na Forodha ya Marekani, hivi karibuni ameonyesha mipango inayoashiria urejeleaji wa vituo vya kukamata familia za wahamiaji. Pia ametangaza kwamba wazazi wasio na nyaraka wa watoto waliozaliwa nchini Marekani, wanapaswa kufanya maamuzi kuhusu kuhifadhi familia.

Trump katika wiki zilizopita pia ameweka msisitizo katika kutekeleza sera yake dhidi ya uhamiaji na ametangaza kuwa atatekeleza operesheni kubwa zaidi ya kuwatimua wahamiaji haramu Marekani.

Yeye hata amezungumzia matumizi ya jeshi katika kutekeleza sera hii, suala ambalo limeibua ukosoaji mwingi na wengi wameona matumizi ya jeshi katika kutekeleza sera hii kuwa ni kinyume cha sheria nchini Marekani.

Maafisa  wa Ofisi ya Wahamiaji na Nidhamu ya Forodha Marekani (ICE) wakiwa wamemkamata mhamiaji haramu

Rais mteule wa Marekani katika taarifa yake ya hivi karibuni amesema kuwa ana mpango wa kutoa amri ya kufuta sheria ya haki ya uraia kwa wanaozaliwa katika ardhi ya Marekani.

Kulingana na sheria ya uraia inayotegemea haki ya kuzaliwa, kila mtu anayezaliwa Marekani bila kujali hali ya uhamiaji ya wazazi wake anaweza kupata uraia wa nchi hii.

Timu ya Trump imeahidi kutekeleza sera za kupambana na uhamiaji, kama vile kubadilisha sheria, kuendelea na mradi wa kujenga ukuta wa mpaka kati ya Marekani na Mexico, matumizi ya teknolojia za kisasa za ufuatiliaji na kuongeza idadi ya wafanyakazi wa forodha na ulinzi wa mpaka na kuingia makubaliano na nchi za tatu ambapo wahamiaji wanaotaka hifadhi wanapaswa kusubiri katika nchi za tatu kama Mexico.

Hata hivyo, mipango hiyo ya Trump itachukua muda mrefu kutekelezwa kutokana na gharama kubwa na ukosefu wa wafanyakazi wa kutosha.

Kwa upande mwingine, wapinzani wengi wa sera hizi, ikiwa ni pamoja na vikundi vya kutetea haki za wahamiaji, huenda wakaleta malalamiko ya kisheria makubwa dhidi ya sera za kupinga wahamiaji za Trump.

Inaonekana Trump licha ya kauli mbiu zote na kuunda timu yenye nguvu iliyo dhidi ya wahamiaji, ana njia ngumu ya kutimiza ahadi ya kufukuza wahamiaji haramu. Atakumbana na vizingiti vya kisheria, watetezi wa haki za binadamu na hata mashirika yanayotumia wahamiaji ambao kwa kawaida huridhia mishahara midogo na hata wakikandamizwa kazini huwa hawana pa kukimbilia.

Popular posts from this blog

Jeshi la Wanamaji la Marekani limesema linakabiliwa na vita 'kali zaidi' tangu Vita vya Pili vya Dunia dhidi ya Wayemeni

Putin asaini mkataba wa kituo cha Mwezi na China