'Niliwaambia wachezaji wa Sudan wajione kama wao ni Messi au Ronaldo'
Wakati Sudan inafuzu Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon 2025), macho yote yaligeukia kazi iliyofanywa na kocha wao mkuu Kwesi Appiah.
Je, Mghana huyo alimudu vipi licha ya hali mbaya ya taifa hilo ambalo limekumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miezi 20?
"Kufuzu Afcon ilikuwa moja ya malengo niliyojiwekea kabla sijatia saini mkataba, kwa hivyo kufanikiwa lilikuwa jambo ambalo lilikuwa moyoni mwangu," Appiah aliambia BBC Sport Africa alipokuwa akitafakari hatua kubwa iliyopigwa.
"Sababu nyingine iliyonifanya nisajili ni kwa ajili ya watu wa Sudan, kwa sababu ya vita huko nyumbani. Wachezaji wameonyesha kujituma sana. Nani ajuaye, labda kupitia kandanda vita vinaweza hata kumalizika. Na hilo lilikuwa jambo ambalo lilinifurahisha."
Tangu mzozo huo uanze mwezi Aprili mwaka jana, wachezaji wa Sudan - wengi wao walioathirika binafsi - hawana makazi ya kudumu. Ligi ya ndani imesimamishwa na mechi za kufuzu nyumbani zimechezwa nchini Libya na nchi jirani ya Sudan Kusini.
Katikati ya mazingira magumu kama haya, Appiah, 64, anasema afya ya kisaikolojia ni muhimu.
"Ninaamini ni suala la kuwapa akili wachezaji wako ili wajisikie kuwa ni (Lionel) Messi au (Cristiano) Ronaldo [ili] mchezo wowote watakaoingia wasijisikie kuwa hakuna kikomo," anaeleza.
"Popote uendapo, mahali hapo ni nyumbani kwetu, iwe tuna mashabiki au hatuna, nenda ukaichezee familia yako, wewe mwenyewe na nchi yako.
"Hili ni jambo ambalo vijana wanaweza kufanya ili kubadilisha vita - au kusimamisha vita - nchini Sudan, kwa kujaribu kufuzu kwenye Afcon au Kombe la Dunia. Angalau nimewapa kitu cha kuangalia na kisha kupigania."
Kandanda 'ufunguo wa amani' katika vita
Mzozo kati ya jeshi la Sudan na wanamgambo wa Rapid Support Forces umewalazimisha zaidi ya watu milioni 11 kukimbia makwao.
Wafanyakazi wa misaada wanasema imesababisha mzozo mbaya zaidi wa kibinadamu duniani - na Appiah amelazimika kutazama baadhi ya wachezaji wake wakipata changamoto hizo.
"Ninajua jinsi Wasudan walivyo na upendo. Wachezaji wanne walipoteza familia zao wakiwa kambini," alisema.
"Ni hali ya kusikitisha sana, lakini wanajaribu kustahimili, wachezaji wote waliwafariji na kuwatia moyo. Haikuwa rahisi. Tunakabiliwa na majeraha haya yote, lakini tunajaribu kustahimili."
Wakihitaji alama moja tu kutoka kwa mechi zao mbili za mwisho za kufuzu kwa fainali za Afcon mwakani, Sudan ilimenyana na Niger katika mechi yao ya mchujo, na kupoteza kwa mabao 4-0.
"Kwa kweli ilikuwa hali ambayo hatukuwahi kutarajia," Appiah alisema. "Wakati wowote hali kama hizi zinatokea, unachohitaji kufanya ni kuweka mchezo nyuma yako. Unajifunza kutokana na hayo, halafu unasonga mbele."
Vijana wa Appiah hawakufanya makosa mjini Benghazi kwenye kizingiti cha mwisho, wakiwabana washindi wa kundi Angola kwa sare ya 0-0 na kufikia kile ambacho wengi walidhani kuwa hakiwezekani.
"Baada ya kufuzu tulikwenda kwenye ubalozi wa Sudan, balozi akasema 'Kila mtu [huko Sudan] alikuwa ameweka bunduki chini, na wote walikuwa wanashangilia mitaani, jambo ambalo si la kawaida kwa sababu ukifika mitaani lazima kuangalia huku na huku [kwa tahadhari] kama bunduki inakulenga," Appiah alisema.
"Hilo ni jambo ambalo huwa nawaambia wachezaji kabla ya mechi yoyote. Angalia jamaa zako, wale wa nyumbani, wanapitia nini, na tuweke tabasamu kwenye nyuso zao. Kandanda ni mojawapo ya funguo zinazoweza kufungua amani dhidi ya vita hivyo."
Ndoto za Kombe la Dunia
Kwa wachezaji wa Sudan, inawezekana kufuzu na kuweka historia kwenye mashindano ya Kombe la Dunia la Fifa.
Baada ya awamu nne za mchujo wa 2026, Falcons of Jediane wanakaa kileleni mwa kundi la timu sita ambalo pia linajumuisha Senegal na DR Congo.
Kampeni itaanza tena Machi, na Appiah anaamini kujiamini ndio silaha yao kuu.
"Angalia timu bora zaidi ulimwenguni - Uhispania, England, Ujerumani au Brazil," alisema.
"Nawaambia [wachezaji]: 'Unawezaje kulenga kwenda Kombe la Dunia kama hutajiweka katika kiwango chao?'"
Mojawapo ya wakati wa kufurahisha zaidi katika harakati zao za kufuzu Kombe la Dunia ilikuwa Juni walipocheza na nchi jirani ya Sudan Kusini - nchi ambayo ilikuwa vitani nayo.
Sehemu kubwa ya umati wa Juba walijiunga na wimbo wa taifa wa Sudan kabla ya mechi hiyo, ambayo Sudan ilishinda 3-0.
Appiah anasema ilileta "umoja kwa kiasi kikubwa" kwa nchi zote mbili.
'Ghana ni kama Uingereza'
Ingawa vita vya nyumbani vimekuwa msingi wa kufuzu kwa Sudan Afcon 2025, matokeo ya Appiah dhidi ya taifa lake la Ghana pia yameteka vichwa vya habari.
Sudan waliwabana Black Stars kwa sare ya 0-0 mjini Accra na kisha kuwafunga 2-0 mjini Benghazi - matokeo ambayo yalichangia Ghana kushindwa kufuzu Kombe la Mataifa kwa mara ya kwanza baada ya miaka 20.
"Ni bahati mbaya sana kwa sababu kila mtu alifikiri Ghana itakuwa imefuzu," Appiah alitafakari.
"Mnamo 2014, nilikuwa nikipeleka Ghana kwenye Kombe la Dunia huko Brazil, na nilitoa taarifa kwamba mpira wa miguu unazeeka.
"FA nzima inahitaji kukaa chini na kuchambua na kuangalia nini kinaendelea."
Appiah anasema alizitaka Sudan na Ghana kufika katika michuano hiyo nchini Morocco, lakini lengo lake lilikuwa kabisa kwa Sudan.
"Nilikuwa mwanachama mtendaji wa FA nchini Ghana na wakati Ghana inashiriki katika kundi letu, niliambiwa nijitoe kwa sababu ya mgongano wa kimaslahi, na nilifanya hivyo.
"Ukishakuwa mtaalamu, unaangalia unapofanya kazi. Kama Ghana haifanyi vizuri kwenye mchuano huo, hakuna ninachoweza kufanya.
"Ninahitaji kuwa mtaalamu 100% na kuhakikisha kuwa nchi ninayofundisha inafuzu [kwa] ama Afcon au Kombe la Dunia."
Appiah pia anamhurumia kocha mkuu wa sasa wa Ghana Otto Addo.
"Ghana ni kama England. Ikiwa England haitafuzu kwa Ulaya au Kombe la Dunia, ni suala kubwa, kubwa," alisema.
"Mara tu unapochukua kazi hiyo, unahitaji kuongeza nguvu kubwa hapo. Ghana kutokwenda Afcon ni jambo kubwa, kubwa, kubwa."