Starehe ya kupiga picha msimu wa likizo
- Author, Mariam Mjahid
- Nafasi, BBC Swahili
Sanaa ya upigaji picha inaegemea sana uwepo wa mwangaza. Bila ya nuru, picha hiyo itakuwa na shaka. Hapo zamani, picha ilikuwa ni nyeupe na nyeusi na sanaa hii ya picha ilisambaa haraka kote duniani.
Kama vile Peter Muriuki, mpiga picha wa miaka ya 1970 anavyotueleza namna picha zilivyoenziwa karne hii hiyo.
“Watu barabarani walikuwa wanaangalia picha kisha wanachagua eneo wanalolipenda, na wanasema niwapigie hapo,” anasema Muriuki.
Kabla ya kuvumbuliwa picha watu walitegemea wachoraji ili kupata picha za wanyama au binadamu, kabla ya ujio wa picha safi bila uchoraji.
Karne hii unaweza kupiga picha kwenye simu yako au tarakilishi. Lakini zamani ilikuwa ni kitu cha kustaajabisha.
Ni vipi unaweza kuhifadhi sura yako unayoiyona kwa kioo?
Uvumbuzi wa kamera
Uvumbuzi ukaanza! Picha ya kwanza ilipigwa kwa kutumia kamera ya obscura.
Mwanafalsa alivumbua kuwa mwanga ukichujwa ukipitia tundu ndogo ya dirisha, kivuli kinachorudia ukutani unaweza kuona mazingira ya nje ya dirisha.
Naye Thomas Wedgewood akagundua kuwa picha hiyo ikipigwa inaweza kuhifadhiwa.
Mwaka 1826, Nicéphore Niépce alifanya mapinduzi katika teknolojia ya upigaji picha kwa kufanikiwa kugandisha picha iliyopigwa na kamera.
Hata hivyo, mchakato huu ulitumia muda mrefu, angalau saa nane na wakati mwingine hata siku kadhaa. Hata hivyo, picha hizo zilikuwa za kudumu, ingawa zilikuwa zinachukua muda.
Dunia ilijulishwa picha ya kwanza mwaka 1839, mwaka ambao unajulikana sana kama kuzaliwa kwa upigaji picha wa kivitendo.
Baada ya habari za 'daguerreotype' kuenea, William Henry Fox Talbot alibuni mchakato wa 'negative-positive' uliohitaji asidi ya inayojulikana kama 'gallic' kwenye karatasi inayoakisi mwanga, na kutoa picha.
Upigaji picha ulianza kuwa rahisi na kubadilika kutokana na maendeleo yaliyofuata.
Uvumbuzi wa vifaa vipya ulipunguza muda kutoka dakika hadi sekunde na hatimaye sehemu za sekunde. Pia, maendeleo ya vifaa vipya vya mwanga vilileta ufanisi zaidi na urahisi.
Mnamo mwaka 1888, George Eastman aligundua filamu inayoviringika na kuzindua kamera ya Kodak. Kamera hii ilikuwa na filamu ya picha 100, na ilichukua picha za duara.
Bei ya awali ya Kodak ilikuwa dola $25, na ilijumuisha filamu na begi la ngozi. Mtu alipotumia filamu yote, kamera ilirejeshwa kiwandani ili picha zichapishwe.
Mapinduzi yalijiri mwaka 1975, wakati Steve Sasson, mhandisi kutoka Eastman Kodak, alipogundua kamera yenye sensa ya chaji, iliyobeba vifaa vya sensor charge-coupled device (CCD).
Sensa yenye uimara chini ya megapixel moja ilipiga picha za rangi za kijivu na kuzihifadhi kwenye kaseti ya sauti. Lakini, hii ilibadilisha historia ya upigaji picha.
Taaluma ya upigaji picha
Peter Muriuki, mwenye umri wa miaka 70 ambaye ni mkaazi wa eneo la Dandora, jijini Nairobi, anaeleza namna taaluma hii ilivyomuunganisha na watu wengi: "Picha ni kitu cha kuvutia, najifunza na inanikutanisha na watu, uzuri ni kazi ya kijamii."
Haikuwa rahisi katika taaluma ya upigaji picha. Walikuwa wakitumia kanda za filamu ambapo ilichukua muda kabla ya kupata nakala ya picha.
“Baada ya wiki mbili, mteja anakuta alifunga macho na unajua wakati huo usingepiga picha nyingi, lakini sasa imekuwa rahisi hata mpiga picha asiyekuwa mtaalamu anaweza kupiga picha,” anasema Muruiki.
Raha ya kupigwa picha
Upigaji picha sasa umechukua mkondo tofauti na wakusisimua. Tafakari ukipiga picha ukiwa umeshikilia jengo refu, ni teknolojia ya sasa lakini inanaswa vipi?
John Muchuri, mpigaji picha anayepatikana katika jumba la mikutano la KICC jijini Nairobi anatuibia siri ya manjonjo hayo.
“Unainua tu mkono unajifanya kama umeshika paa la jengo hilo kisha tukinasa picha hiyo tutaifanyia ukarabati, picha itajitokeza umeshikilia jengo hilo watu wanafurahia sana aina hii ya picha.”
Wapiga picha ambao hufurika hapa wanasema taaluma ya upigaji picha inalipa. Lakini hunoga zaidi msimu wa likizo haswa krismasi na mwaka mpya.
‘Kuna watu bado hawajafika jiji kuu la Nairobi na wanapozuru wanakuja kupiga picha kama vile alivyoona mwenzao, hivyo ndo mambo hukua,” anasema Muchuri.
Ujio wa "Selfie"
Ujio wa simu za mikononi ambazo zina kamera hazijawababaisha na kukatiza biashara zao.
"Watu wana simu lakini ubora w simu zao uko chini, tunawapiga kwa kamera zetu kisha tunawaekea kwa simu zao.''
Mpiga picha wa BBC, anasema upigaji picha ni daraja la kuunganisha asiria na asilia.
Teknolojia inavyoendelea kubadilika watu haswa wapenzi wa mitandao ya kijamii wanajipiga picha wenyewe au kupiga picha kupitia kioo almaarufu selfie. Mtindo huu wa kupiga picha wa selfie ukawekwa katika kamusi ya 2013.
Wakenya haswa wasanii wa maudhui katika jukwaa la Tiktok wametambua kuwa ukipiga picha lazima, uiendane na mazingira yatakayosawiri maudhui.
Vijana wa Afrika mashariki wameanza kujiganga na kujieleza kupitia sanaa ya upigaji picha baada ya mitandao ya kijamii kuwa kitega uchumi kwa wengi.
Peter Njoroge ambaye ni mpiga picha wa BBC, anaeleza kuwa awali taaluma ya upigaji picha ilikuwa inadidimia lakini sasa mambo yanabadilika.
Akitoa mfano kuwa ingawa watu sasa wana simu zina kamera wameanza kupendelea kupigwa picha na kamera zikionyesha mandhari ya nyuma yakiwa tofauti.
"Zamani kulikuwa na picha za filamu kisha kukaja kamera za kidijitali na simu zilizo na kamera zikafuata, ikawa watu wanajipiga picha wanavyotaka bila kuhitaji wanaopiga picha. Sasa vijana pale mjini wanajieka sehemu fulani na wameelewa namna ya kupiga picha, ambayo huko nyuma huoni mazingira vizuri lakini ukijiangalia wewe unaonekana vizuri. Hilo limeleta mwamko mpya sasa, watu wanatoroka tena picha za simu wanakwendea zile za dijitali kwasababu zina umaridadi wake kwa macho."
Na kuhusu siku za baadaye za taaluma ya upigaji picha, mpigaji picha wa BBC ananukuu msemo wa kuwa “picha huzungumza maneno 1000, picha bado zitaendelea na zina ukweli wake hata kama kuna mtindo wa kuzihariri, ila picha bado ina maisha."