Biden kutuma shehena ya silaha kwa Israel
Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imearifu Bunge la Congress kuhusu mpango wa kuiuzia Israel silaha kwa thamani ya $8bn (£6.4bn), afisa wa Marekani ameithibitishia BBC.
Shehena ya silaha, ambayo inahitaji idhini kutoka kwa kamati za Bunge na Seneti, inajumuisha makombora na silaha nyingine.
Hatua hiyo inajiri takribani wiki mbili kabla ya Rais Joe Biden kuondoka madarakani.
Washington imekataa wito wa kusitisha msaada wa kijeshi kwa Israel kwa sababu ya idadi ya raia waliouawa wakati wa vita huko Gaza.
Mwezi Agosti, Marekani iliidhinisha uuzaji wa ndege za kivita zenye thamani ya $20bn na vifaa vingine vya kijeshi kwa Israel.
Mpango wa Shehena ya hivi karibuni ina makombora ya kutoka angani na mabomu, afisa huyo wa Marekani alisema.
Chanzo kimoja kinachofahamu mauzo hayo kiliiambia BBC siku ya Jumamosi: "Rais ameweka wazi kuwa Israel ina haki ya kutetea raia wake, kwa kuzingatia sheria za kimataifa za kibinadamu, na kuzuia uchokozi kutoka kwa Iran na washirika wake.
"Tutaendelea kuwezesha kila msaada unaohitajika kwa ulinzi wa Israel."
Biden mara nyingi ameelezea kuhusu kuiunga mkono Israel bila kutetereka.
Marekani ndiyo muuzaji mkuu zaidi wa silaha kwa Israel, baada ya kuisaidia kujenga mojawapo ya jeshi lililobobea zaidi kiteknolojia duniani.
Kwa mujibu wa Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Amani ya Stockholm (SIPRI), Marekani ilichangia 69% ya silaha kuu za Israeli kati ya 2019 na 2023.