Elon Musk akosolewa kwa kutoa taarifa za uongo kuhusu magenge ya wabakaji
Ukosoaji wa Elon Musk dhidi ya serikali ya Uingereza namna inavyoshughulikia magenge ya wabakaji “sio sahihi na ni upotoshaji," amesema Katibu wa masuala ya Afya, Wes Streeting.
Bilionea Musk amechapisha msururu wa taarifa kwenye tovuti yake ya kijamii ya X, akimshutumu Waziri Mkuu wa Uingereza, Sir Keir Starmer kwa kushindwa kushughulikia magenge ambayo yaliwabaka wasichana wadogo, na kutaka waziri wa ulinzi Jess Phillips afungwe jela.
Alipoulizwa kuhusu maoni hayo, Streeting alisema "serikali hii inachukulia suala la unyanyasaji wa kijinsia kwa watoto kwa umakini mkubwa."
Amemwalika Musk "kujitayarisha na kufanya kazi nasi" dhidi ya magenge ya ubakaji.
Kiongozi wa Conservative, Kemi Badenoch ametoa wito wa uchunguzi kamili kuhusu kile alichokiita "kashfa ya magenge ya ubakaji" Uingereza.
Lakini chama hicho pia kimemkosoa Musk kwa "kuchapisha taarifa ambazo sio sio sahihi" na kujitenga na wito wake wa kutaka Phillips afungwe.