Ghana yazindua visa ya bila malipo kwa Waafrika wote
Wamiliki wote wa pasipoti wa Kiafrika sasa wanaweza kuzuru Ghana bila kuhitaji visa, Rais anayemaliza muda wake Nana Akufo-Addo amesema.
Alitangaza mpango huo mwezi uliopita lakini katika hotuba yake ya mwisho ya hali ya taifa siku ya Ijumaa alisema kuwa sera hiyo ilianza kutekelezwa mwanzoni mwa mwaka.
Usafiri bila visa ndani ya bara kwa muda mrefu umekuwa hamu kwa wale wanaokuza maadili ya Uafrika na inaonekana kuwa muhimu kwa ushirikiano wa kiuchumi.
Ghana sasa ni nchi ya tano barani Afrika kutoa hii kwa wasafiri kutoka bara zima.
Nchi nyingine ni Rwanda, Ushelisheli, Gambia na Benin.
"Ninajivunia kuidhinisha safari bila viza kwenda Ghana kwa wamiliki wote wa pasipoti wa Kiafrika, kuanzia mwanzoni mwa mwaka huu," Akufo-Addo aliwaambia wabunge katika hotuba yake ya mwisho bungeni kabla ya kujiuzulu wiki ijayo baada ya miaka minane mamlakani.