Israel imethibitisha kuwa inamshikilia mkuu wa hospitali ya Gaza Abu Safiya
Israel imethibitisha kuwa inamshikilia mkurugenzi wa hospitali ya Gaza Dr Hussam Abu Safiya baada ya hapo awali kuliambia shirika lisilo la kiserikali la eneo hilo kuwa halina taarifa zake, na hivyo kuzua wasiwasi kuhusu afya yake.
Taarifa ya Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) ilisema "kwa sasa anachunguzwa na vikosi vya usalama vya Israel" ana kwa ana.
Taarifa hiyo haikutoa ufafanuzi kuhusu mkanganyiko huo lakini ilisisitiza kwamba anashukiwa kuwa "gaidi" anayeshikilia cheo" katika kundi la Hamas, Wapalestina wenye silaha wanalopigana na Israel huko Gaza.
Dk Abu Safiya alikamatwa wakati jeshi la Israeli likiwalazimisha wagonjwa na wafanyikazi wa afya kuondoka katika hospitali ya Kamal Adwan kaskazini mwa Gaza Ijumaa iliyopita, kwa madai kuwa kituo hicho ni "ngome ya magaidi wa Hamas".
Siku ya Alhamisi IDF iliwaambia Madaktari wa shirika la kutetea Haki za Kibinadamu Israel (PHRI) kwamba "haijamkamata wala kumshikilia mtu huyo".
PHRI iliwasilisha ombi katika Mahakama Kuu ya Israel siku ya Alhamisi, ikitaka kufahamishwa mahali alipo Dkt Abu Safiya kufichuliwa. Ilisema mahakama iliipa IDF wiki moja kutekeleza.
Wakati huo huo mkuu wa Amnesty Agnès Callamard alisema mamlaka ya Israel lazima "ifichue haraka aliko".
Alisema Israel imewazuilia "mamia ya wahudumu wa afya wa Kipalestina kutoka Gaza bila kufunguliwa mashitaka" na kusema "wameteswa na kutendewa vibaya na kuzuiliwa bila mawasiliano".
Hata hivyo Israel inakanusha kuwatesa wafungwa.
Awali familia ya Dkt Abu Safiya iliambia Idhaa ya Kiarabu ya BBC kwamba wanaamini anazuiliwa katika kambi ya kijeshi ya Sde Teiman kusini mwa Israel, ambapo majeshi ya Israel yamewachukua wafungwa wengi kutoka Gaza kwa mahojiano.
Hapo awali wafichuaji waliambia BBC na vyombo vingine vya habari vya kimataifa kuhusu hali ngumu sana inayowakabili wafungwa walioko.
Israel imesema wafungwa wote huko wanahifadhiwa "kwa uangalifu na ipasavyo".
IDF iliamuru kila mtu ndani ya hospitali ya Kamal Adwan kuondoka Ijumaa iliyopita asubuhi, na kutoa muda wa takribani dakika 15 kwa hospitali hiyo kuwahamisha wagonjwa na wafanyikazi ndani ya eneo hilo, wahudumu wa afya waliambia BBC.
Mji wa Beit Lahia, iliko hospitali hiyo umekuwa chini ya vizuizi vikali vya Israel vilivyowekwa kwenye maeneo ya kaskazini mwa Gaza tangu Oktoba.
Umoja wa Mataifa umesema eneo hilo limezingirwa kwa karibu huku jeshi la Israel likizuia kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa misaada katika eneo hilo ambalo wastani wa watu 10,000 hadi 15,000 wamesalia.
Siku ya Jumamosi, IDF ilisema iliwakamata wapiganaji 240 huko Kamal Adwan na kusema Dk Abu Safiya alikuwa miongoni mwa wafanyikazi wa afya waliochukuliwa kuhojiwa.
Picha za video zilimuonyesha akitembea kuelekea kwenye gari la kivita la Israel kabla ya kupelekwa kuhojiwa. Msemaji wa jeshi la Israel alithibitisha kukamatwa siku hiyo hiyo, akisema daktari huyo alikuwa amehamishwa kwa ajili ya kufanyiwa mahojiano.
Dk Abu Safiya hapo alikamatwa na vikosi vya Israel wakati wa uvamizi wa awali katika hospitali hiyo mwezi Oktoba, lakini aliachiliwa muda mfupi baadaye. Wakati wa operesheni hiyo ya Israel mtoto wa kiume wa Dkt Abu Safiya mwenye umri wa miaka 15 aliuawa katika shambulio la ndege zisizo na rubani. Picha za baadaye siku hiyo zilimuonyesha akiongoza dua ya mazishi ya mwanawe katika eneo la hospitali.
Mashambulizi ya Israel dhidi ya vituo vya afya vya Gaza yamesababisha kulaaniwa zaidi.
Siku ya Jumanne Ofisi ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa ilisema mashambulizi ya Israel katika hospitali na kandokando ya hospitali yamechangia kuharibu mfumo wa afya wa Gaza kabisa" na kuibua wasiwasi mkubwa kuhusu uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu.
Ujumbe wa Israel mjini Geneva ulisema vikosi vya Israel vinafanya kazi kwa mujibu wa sheria za kimataifa na "kamwe havitalenga raia wasio na hatia".
Israel ilianzisha kampeni ya kuiangamiza Hamas kujibu mashambulizi ya kundi hilo,mashambulizi ambayo hayajawahi kushuhudiwa kusini mwa Israel tarehe 7 Oktoba 2023, ambapo takriban watu 1,200 waliuawa na wengine 251 walichukuliwa mateka.
Zaidi ya watu 45,580 wameuawa huko Gaza tangu wakati huo, kulingana na wizara ya afya ya eneo hilo.