Msamaha wa familia ya muathirika: Tumaini pekee kwa muuguzi wa India anayesubiri kunyongwa nchini Yemen
Wanafamilia wa muuguzi wa Kihindi ambaye anasubiri kunyongwa katika nchi ya Yemen iliyokumbwa na vita wanasema wanaweka matumaini yao katika juhudi za mwisho za kumwokoa.
Nimisha Priya, 34, alihukumiwa kifo kwa mauaji ya mwanamume wa eneo hilo - mshirika wake wa zamani wa biashara Talal Abdo Mahdi - ambaye mwili wake uliokatwakatwa uligunduliwa kwenye tanki la maji mnamo 2017.
Akiwa katika jela kuu la mji mkuu Sanaa, anatazamiwa kunyongwa hivi karibuni, huku Mahdi al-Mashat, rais wa Baraza Kuu la Kisiasa la waasi wa Kihouthi, akiidhinisha adhabu yake wiki hii.
Chini ya mfumo wa mahakama ya Kiislamu, unaojulikana kama Sharia, njia pekee ya kukomesha unyongaji sasa ni kupata msamaha kutoka kwa familia ya muathiriwa.
Kwa miezi kadhaa, jamaa na wafuasi wa Nimisha wamekuwa wakijaribu kufanya hivi kwa kuchangisha diyah, au pesa ya damu, ili kulipwa kwa familia ya Mahdi, na mazungumzo yamekuwa yakiendelea.
Lakini baada ya muda kuisha, wafuasi wanasema matumaini yao yanategemea kabisa uamuzi wa familia.
Chini ya sheria za Yemen, familia ya Nimisha haiwezi kuwasiliana moja kwa moja na familia ya muathirika na lazima iajiri wanaofanya mazungumzo.
Subhash Chandran, wakili ambaye ameiwakilisha familia ya Nimisha nchini India siku za nyuma, aliiambia BBC kwamba familia hiyo tayari ilikuwa imefadhilisha $40,000 (£32,268) kwa ajili ya familia ya muathiriwa.
Pesa hizo zimetolewa kwa awamu mbili kwa mawakili walioajiriwa na serikali ya India ili kujadili kesi hiyo (kucheleweshwa kwa kupeleka awamu ya pili kuliathiri mazungumzo, Bw Jerome anasema).