Mtu mwenye umri mkubwa zaidi duniani Tomiko Itooka afariki akiwa na umri wa miaka 116
Mwanamke wa Kijapani, anayetambuliwa kama mtu mzee zaidi duniani na Guinness World Records, amefariki akiwa na umri wa miaka 116.
Tomiko Itooka alifariki katika makazi ya wazee katika jiji la Ashiya, Mkoa wa Hyogo, kulingana na maafisa.
Alikua mtu mzee zaidi ulimwenguni baada ya Maria Branyas Morera wa Uhispania kufariki mnamo Agosti 2024 akiwa na umri wa miaka 117.
"Bi Itooka alitupa ujasiri na matumaini kupitia maisha yake marefu," meya wa Ashiya mwenye umri wa miaka 27 Ryosuke Takashima alisema katika taarifa.
"Tunamshukuru kwa hilo."
Bi Itooka alizaliwa Mei 1908 - miaka sita kabla ya Vita vya Kwanza vya Dunia na mwaka huo huo gari la Ford Model T lilizinduliwa nchini Marekani.
Alithibitishwa kuwa mtu mzee zaidi duniani mnamo Septemba 2024 na akakabidhiwa cheti rasmi cha GWR katika sikukuu ya kuheshimu wazee, ambayo ni sikukuu ya umma ya Japani inayoadhimishwa kila mwaka ili kuwaenzi wazee wa nchi hiyo.
Bi Itooka, ambaye alikuwa mmoja wa ndugu watatu, aliishi na alishuhudia vita vya dunia na magonjwa ya milipuko pamoja na mafanikio ya kiteknolojia.
Akiwa mwanafunzi, alicheza mpira wa wavu na kupanda Mlima Ontake wa mita 3,067 (futi 10,062) mara mbili.
Katika umri wake, alifurahia ndizi na Calpis, kinywaji baridi cha maziwa maarufu nchini Japani, kulingana na taarifa ya meya.
Aliolewa akiwa na umri wa miaka 20, na alikuwa na binti wawili na wana wawili wa kiume, kulingana na Guinness.
Wakati wa Vita vya Pili vya Ulimwengu alisimamia ofisi ya kiwanda cha nguo cha mumewe. Aliishi peke yake huko Nara baada ya mumewe kufariki mnamo 1979.
Ameacha mtoto mmoja wa kiume na wa kike mmoja na wajukuu watano. Ibada ya mazishi iliandaliwa na familia na marafiki, kulingana na maafisa.
Kufikia Septemba, Japan ilihesabu zaidi ya watu 95,000 ambao walikuwa umri wa miaka 100 au zaidi na 88% kati yao walikuwa wanawake.