Mufti wa Oman atoa mwito wa kuungwa mkono mashujaa wa Yemen
Mufti Mkuu wa Oman amewataka watu wenye mwamko na waungwana wa Yemen na mataifa yote huru duniani kuwahami na kuwaunga mkono mashujaa wa Yemen ambao wamesimama imara kwenye njia ya haki ya kupambana na madhalimu.
Sheikh Ahmad bin Hamad al-Khalili ametoa mwito huo na kusema: "Wanamapambano mashujaa wa Yemen wanaendelea kupigania haki na kupambana na madhalimu kwa ushujaa na azma isiyo na kifani ambayo inatikisa milima na mawe yenye nguvu."
Ameongeza kuwa: "Kama ambavyo ni wajibu kwa kila raia muungwana wa Yemen kuungana na mashujaa hao na kuimarisha Muqawama wao hadi kufikia malengo yao matakatifu, ni hivyo hivyo Umma wote wa Kiislamu lazima uwaunge mkono kwa nguvu zao zote mashujaa hao kwa sababu hii ni haki ya Waislamu wote na ni kama Mtume SAW alivyosema: Waislamu wote ni ndugu, hawadhulumiani na wala hawasababishiani matatizo."
Mwishoni mwa matamshi yake, Mufti Mkuu wa Oman amesema: Majeshi ya Muqawama yanajitolea muhanga kwa ajili ya taifa la Palestina, hivyo na mataifa yote ya Kiislamu lazima yashirikiane na yapeane ulinzi wakati yanapotokea mashambulizi ya adui dhidi ya nchi yoyote, zikiwemo ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni ambako ndiko kiliko Kibla cha Kwanza cha Waislamu na ndiko ambako Mtume wetu Muhammad SAW alipaa kwenda mbinguni katika kisa cha Miiraj.
Amesema: "Waislamu wanapaswa kujitahidi kurudisha tunu hizo takatifu kwa mikono safi na yenye ikhlasi ya Umma wa Kiislamu. Hivyo tunaomba mataifa na watu wote wenye dhamiri na fikra uhuru walisimamie jambo hili na wasipuuze wajibu huu mtukufu na Mungu Ndiye Msaidizi wa waliodhulumiwa."