Sababu za Serikali ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina kufuata muelekeo sawa na wa utawala wa Kizayuni dhidi ya HAMAS
Serikali ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina imeendelea kufuata muelekeo sawa na wa utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS kwa kutoa amri ya kufungwa Chaneli ya Televisheni ya Al Jazeera ya Qatar huko Ramallah.
Siku ya Jumatano usiku, Mamlaka ya Ndani ya Palestina
ilitangaza kuwa imepiga marufuku shughuli za Al Jazeera kwa sababu ya
ilichokiita "kukiuka sheria na kanuni za ndani na kutangaza maudhui za
kichochezi".
Kutokana na uamuzi huo, shughuli zote za ofisi ya Al Jazeera ndani
ya Palestina, ikiwa ni pamoja na utangazaji wa vipindi na shughuli za
wanahabari na maripota wa chaneli hiyo zimesimamishwa.
Hatua hiyo iliyochukuliwa na Mamlaka ya Ndani ya Palestina inaweza kuchambuliwa kwa kuzingatia nukta kadhaa.
Kwanza ni kuwa, hatua hiyo imechukuliwa wakati kabla ya
hapo, utawala wa Kizayuni nao pia ulishaipiga marufuku Al Jazeera
kutangaza katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu zilizopachikwa jina
bandia la Israel. Kwa hivyo, kilichofanywa na Mamlaka ya Ndani ni
muendelezo wa harakati za utawala wa Kizayuni dhidi ya Muqawama wa
Palestina hususan Hamas. Hivi karibuni, na katika hatua inayofuata
muelekeo wa utawala wa Kizayuni dhidi ya Hamas, Mamlaka ya Ndani ya
Palestina iliwatia mbaroni na kuwaweka kizuizini wanachama wa Hamas, na
ikamuua shahidi pia kwa kumpiga risasi mwandishi mmoja wa habari
iliposhambulia mikusanyiko ya watu hususan katika mji wa Jenin.
Nukta nyingine muhimu ni kwamba, Mamlaka ya Ndani ya Palestina
imesimamisha shughuli za Al Jazeera huko Ramallah katika hali ambayo,
televisheni hiyo ni miongoni mwa vyombo vichache vya habari katika eneo
vinavyoakisi jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya Ghaza; na kwa kufanya
hivyo, imeukasirisha na kuughadhibisha utawala huo ghasibu. Na ni kwa
sababu hiyo pia, ndio maana Harakati ya Jihadul-Islami ya Palestina
imetoa taarifa, ambayo mbali ya kuikosoa Mamlaka ya Ndani ya Palestina
kwa kusimamisha shughuli za Al Jazeera mjini Ramallah, imesisitiza kuwa,
hatua hiyo inakinzana na muelekeo wa vuguvugu la umma kimataifa la
kuwatetea Wapalestina na kulaani jinai za utawala wa Kizayuni.
Jihadul-Islami imeongezea kwa kusema, kuifungia Al Jazeera isiendeshe
shughuli zake kwa visingizio vya kisiasa, kutapelekea kufichika mauaji
ya kimbari yanayofanywa na utawala wa Kizayuni na kutoakisiwa na vyombo
vya habari.
Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS, nayo pia imetoa taarifa ikisema, uamuzi wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina wa kuipiga marufuku Televisheni ya Al Jazeera ni ukiukaji wa uhuru wa kutoa maoni na ni hatua ya kukandamiza uhuru wa vyombo vya habari, ambayo inalenga kunyamazisha sauti kinzani na kudhoofisha haki na uhuru wa wananchi, ndani ya Palestina.
Hamas imeuelezea uamuzi huo kuwa ni sehemu ya mfululizo wa hatua
zinazochukuliwa kiholela na Mamlaka ya Ndani na kusisitiza kwamba,
uamuzi huo ambao si wa kisheria, umechukuliwa katika mazingira nyeti na
hasasi yanayohitajia zaidi kuliko wakati wowote ule, kuakisiwa habari
huru, sahihi na zisizo za upendeleo kuhusu jinai za kinyama zinazofanywa
na utawala wa Kizayuni.
Nukta nyingine ni kwamba, inavyoonekana, Mamlaka ya Ndani ya
Palestina inazitumia jinai na mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala
wa Kizayuni huko Ghaza kama fursa ya kujipatia maslahi ya kisiasa
kwa makundi ya Muqawama wa Palestina na vilevile kama fursa ya kuinua
nafasi yake ya kisiasa. Na hii ni katika hali ambayo, hatua za kiusalama
na dhidi ya vyombo vya habari unazochukua Mamlaka ya Ndani ya Palestina
dhidi ya makundi ya Muqawama zinaweza kusababisha makabiliano na
mapigano ya ndani baina ya Wapalestina badala ya kuinua na kuboresha
nafasi ya kisiasa ya mamlaka hiyo. Suala hili limebainishwa pia katika
taarifa ya Harakati ya Jihadul-Islami ya Palestina; na harakati
hiyo imeionya Mamlaka ya Palestina juu ya kutokea fitna za ndani yakiwa
ni matokeo ya hatua ya mamlaka hiyo kufuata mkumbo na muelekeo wa
kiuadui wa utawala wa Kizayuni.../