Trump kuhukumiwa kwa kutoa pesa kuzuia taarifa, lakini jaji aashiria kuwa hatafungwa jela
Jaji ameamuru kwamba Donald Trump atahukumiwa Januari 10 katika kesi yake ya fedha mjini New York - chini ya wiki mbili kabla ya kuapishwa kuwa rais.
Jaji wa New York Juan Merchan aliashiria kuwa hatamhukumu Trump kifungo cha jela, mashtaka au faini, lakini badala yake "atamuachilia bila masharti", na akaandika kwamba rais mteule anaweza kufika mahakamani binafsi au kwa njia ya mtandao kwa ajili ya kusikilizwa.
Trump alijaribu kutumia ushindi wake wa urais ili kesi dhidi yake ifutwe.
Rais mteule amechapisha kwenye mitandao ya kijamii akitupilia mbali amri ya jaji huyo kama "shambulio la kisiasa lisilo halali" na kuiita kesi hiyo kuwa "hakuna chochote isipokuwa ni wizi wa kura".
Trump alipatikana na hatia mwezi Mei kwa makosa 34 ya kughushi rekodi za biashara zinazohusiana na malipo ya $130,000 (£105,000) kwa nyota wa filamu za watu wazima Stormy Daniels.
Mashtaka yanayohusiana na majaribio ya kuficha malipo kwa mwanasheria wake wa zamani, Michael Cohen, ambaye katika siku za mwisho za kampeni za uchaguzi wa 2016 alimlipa pesa nyota huyo wa filamu za watu wazima ili kukaa kimya kuhusiana na madai ya kukutana na Trump.
Rais mteule amekana kufanya makosa yote na kusema kuwa hana hatia, akidai kuwa kesi hiyo ilikuwa jaribio la kudhuru kampeni yake ya urais mwaka 2024.
Katika makala yake kwenye mtandao wake wa kijamii wa Truth siku ya Jumamosi Trump alisema amri ya jaji "inakwenda kinyume na katiba yetu na, ikiwa itaruhusiwa, itakuwa mwisho wa urais kama tunavyojua".
Msemaji wa Trump Steven Cheung awali aliita amri hiyo kuwa sehemu ya "hila".