Uchunguzi wa jinai za askari wa Uingereza; ni wa kweli au kiini macho?


  • Uchunguzi wa jinai za askari wa Uingereza; ni wa kweli au kiini macho?

Gazeti la The Guardian limeandika kuwa, Wizara ya Ulinzi ya Uingereza imetangaza kuwafungulia mashtaka askari 9 wa kikosi maalumu cha jeshi la nchi hiyo kwa tuhuma za kufanya jinai za kivita nchini Syria na kwamba limeanzisha uchunguzi wa kimahakama dhidi ya mwanajeshi mwingine kwa tuhuma za kufanya jinai nchini Afghanistan.

Gazeti la The Times pia limethibitisha habari ya kufunguliwa mashtaka wanajeshi wa Uingereza, na kutangaza kuwa wanajeshi watano wa kikosi maalumu cha jeshi la nchi hiyo kinachojulikana kwa jina la SAS wanatuhumiwa kufanya uhalifu wa kivita nchini Syria zaidi ya miaka 2 iliyopita, na huenda wakafunguliwa mashtaka katika mahakama ya kijeshi. Wanajeshi hawa wanatuhumiwa kumuua mtu asiye na hatia ambaye walimtaja kuwa mlipuaji wa kujitoa mhanga. Lakini kwa mujibu wa gazeti la Daily Mail, mtu huyo hakuwa amevaa fulana ya kujilipua kwa bomu wakati alipopigwa risasi na kuuawa.

Askari wa Uingereza na Marekani walifanya uhalifu mwingi wa kivita Afghanistan.

Hii si mara ya kwanza kwa jeshi la Uingereza, kama ilivyo Marekani na hata Ujerumani, kutangaza kwamba limetambua na kuwafungulia mashtaka wanajeshi waliofanya uhalifu nchini Afghanistan, Syria au Iraq. Hapo awali, kulichapishwa mamia ya ripoti na malalamiko kuhusu vitendo vya uhalifu vya askari wa Uingereza nchini Afghanistan na Iraq, lakini serikali ya Uingereza na Wizara ya Ulinzi ya nchi hiyo wanajaribu kuficha uhalifu huo.

Uchunguzi halisi wa jinai zilizofanywa na askari wa nchi hizo hususan huko Afghanistan, unaonyesha kuwa, kiasi na jinsi ya jinai zao ni kubwa na za kutisha mno kadiri kwamba jinai kubwa zilizofanywa na wahalifu katika historia ya binadamu zinaonekana si lolote si chochote. Ingawa habari nyingi kuhusu jinai za askari wa Uingereza au Marekani nchini Afghanistan hazijachapishwa kwa uwazi, lakini uvujaji wa baadhi ya habari unaonyesha kuwa, askari hao wahalifu walianzisha jela za kibinafsi nchini Afghanistan, na mbali na kuwasulubu raia wa nchi hiyo kwa aina mbalimbali za mateso ya kimwili na kiakili, walikuwa wakishindana kuua idadi kubwa zaidi ya raia nchini Afghanistan. Kukata vidole vya maiti, kuvamia nyumba za watu nyakati za usiku, kukashifu mila na desturi za kidini za watu wa Afghanistan, kuwakamata watu kiholela na kuchoma moto kitabu kitakatifu cha watu wa nchi hiyo, yaani Qur'ani Tukufu, ili kuwapa mashinikizo na mateso ya kisaikolojia, ni miongoni mwa mienendo isiyo ya binadamu ya askari wa Uingereza na Marekani katika nchi walizozikalia kwa mabavu kama vile Afghanistan.

Pamoja na haya yote, msemaji wa jeshi la Uingereza amedai jeshi la nchi hiyo lina mienendo ya viwango vya ya juu zaidi. Hata hivyo, madai haya yanakadhibishwa na jinai za kutisha zilizofanywa na jeshi la Uingereza katika makoloni na maeneo yote yaliyokalia kwa mabavu na nchi hiyo. Kwa kuzingatia hayo yote, swali la msingi ni kwamba je, tangazo la kufunguliwa mashtaka dhidi ya askari wahalifu wa Uingereza ni la kweli? Na je, wahalifu hao wataadhibiwa?

Askari wa Marekani wakivamia nyumba ya raia, Afghanistan

Tunapoangalia kesi nyingine za kufunguliwa mashtaka askari watendajinai wa Uingereza au Marekani tunaona kuwa, kuchapisha ripoti kama hizo ni hatua ya kimaonyesho tu ya kupotosha fikra za watu na kutaka kuonesha sura ya "ubinadamu" ili kusafisha sura mbaya wa majeshi yao; Kwa sababu mpaka sasa vyombo vya mahakama vya wavamizi hao waliozikalia kwa mabavu nchi za Afghanistan, Iraq na Syria ama havijatoa hukumu dhidi ya askari wa nchi hizo waliotenda jinai na uhalifu au kama wamehukumiwa basi hawajaadhibiwa kivitendo.

Wakati huo huo, kuchapishwa kwa baadhi na ripoti za kujiua baadhi ya askari wahalifu wa Uingereza au Marekani kutokana na matatizo ya akili na mateso ya dhamiri zinazowasuta, kunaonyesha ukubwa wa uhalifu wa askari hao ambao wameshindwa kustahamili na kuamua kujiua.



Popular posts from this blog

Jeshi la Wanamaji la Marekani limesema linakabiliwa na vita 'kali zaidi' tangu Vita vya Pili vya Dunia dhidi ya Wayemeni

Putin asaini mkataba wa kituo cha Mwezi na China