Ukungu watatiza shughuli za maisha na usafari India
Ukungu mzito umetanda Delhi na maeneo ya kaskazini mwa India, na kusababisha changamoto za ucheleweshaji wa safari na taharuki.
Zaidi ya safari 100 za ndege zilicheleweshwa katika uwanja wa ndege wa Delhi siku ya Ijumaa asubuhi, kwa mujibu wa shirika la habari la PTI. Mamia ya safari za garimoshi pia zimepangwa upya, au kuchelewa.
Mamlaka ya hali ya hewa nchini India imesema kuwa hali ya ukungu huenda ikaendelea kwa siku chache zijazo.
Ukungu mzito ni kawaida katika kipindi hiki cha mwaka huko Delhi na maeneo mengine ya kaskazini mwa India, wakati eneo hilo likikabiliwa na wimbi la baridi kali.
Picha na video zilionyesha miji kadhaa iliyogubikwa na ukungu mzito.
Takriban viwanja vya ndege tisa kikiwemo kile cha Delhi vimeripotiwa kutoonekana vizuri Ijumaa asubuhi, Idara ya Hali ya Hewa ya India (IMD) ilisema.
Uwanja wa ndege wa Delhi umetoa ushauri kwa abiria, na kuwataka kuchukua tahadhari kutokana na kuahirishwa kwa safari.
"Wakati kutua na kupaa kukiendelea kwenye uwanja wa ndege wa Delhi, safari za ndege ambazo hazifuati mfumo wa CAT III zinaweza kuathiriwa," taarifa ya uwanja wa ndege ilieleza ikirejelea mfumo wa rada ambao huwezesha kutua wakati kuna muonekano hafifu sana.
Mashirika kadhaa ya ndege pia yametoa taarifa kuwataka wasafiri kuangalia ratiba za ndege kabla ya kupanga safari zao.
IMD inachukulia hali ya ukungu kuwa "mzito" ikiwa mwonekano unapungua chini ya 200m na "mzito sana" ikiwa utashuka chini ya 50m.
Idara ya hali ya hewa imesema kuwa Delhi inaweza kupata mvua nyepesi hadi wastani mnamo 6 Januari, ambayo huenda ikapunguza zaidi joto.