Vikosi vya Guatemala vyawasili Haiti kupambana na magenge ya uhalifu
Kikosi cha wanajeshi 150 wa Guatemala kimewasili Haiti, kikiwa na jukumu la kusaidia kurejesha utulivu huku kukiwa na machafuko yanayotekelezwa na magenge yenye silaha.
Kundi la kwanza la wanajeshi 75 liliwasili siku ya Ijumaa na wengine 75 Jumamosi, wote wakiwa wamesajiliwa kutoka Wizara ya polisi wa kijeshi, kulingana na serikali ya Guatemala.
Hali ya hatari imekuwa ikitanda katika taifa hilo la Caribean kwa miezi kadhaa huku serikali ikipambana na magenge ya kikatili ambayo yamedhibiti sehemu kubwa ya mji mkuu wa Port-au-Prince.
Vikosi hivyo viko nchini Haiti ili kuimarisha kikosi cha usalama kinachoungwa mkono na Umoja wa Mataifa kinachoongozwa na Kenya ambacho hadi sasa kimeshindwa kuzuia ghasia.
Kenya ilituma karibu maafisa 400 wa polisi mwezi Juni na Julai mwaka jana kusaidia kupambana na magenge hayo.
Hiki kilikuwa ni awamu ya kwanza ya kikosi cha kimataifa kilichoidhinishwa na Umoja wa Mataifa ambacho kitaundwa na maafisa 2,500 kutoka nchi mbalimbali.
Idadi ndogo ya vikosi kutoka Jamaica, Belize na El Salvador pia viko Haiti kama sehemu ya mpango huo ambao mfadhili mkuu ni Marekani.
Mnamo Machi 2024, magenge yenye silaha yalivamia magereza makubwa mawili ya Haiti, na kuwaachia huru wafungwa 3,700.
Eneo la Ouest - ikiwa ni pamoja na Port-au-Prince - awali ziliwekwa chini ya hali ya hatari tarehe 3 Machi, baada ya ghasia zinazozidi kushika mji mkuu.
Unaweza kusoma;