Ivory Coast yatangaza kuondoka kwa wanajeshi wa Ufaransa katika taifa hilo la Afrika Magharibi
Chanzo cha picha, AFP Maelezo ya picha, Wanajeshi wa Ufaransa walisaidia kuwalinda raia wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Ivory Coast kuanzia 2002-07 Ivory Coast imetangaza kuwa wanajeshi wa Ufaransa wataondoka katika taifa hilo la Afrika Magharibi, na hivyo kupunguza zaidi ushawishi wa kijeshi wa mkoloni huyo wa zamani katika eneo hilo. Katika hotuba ya mwisho wa mwaka, Rais wa Ivory Coast, Alassane Ouattara, alisema hatua hiyo ni kielelezo cha jeshi la kisasa la nchi hiyo. Nchi jirani ya Senegal, ambayo mwezi uliopita ilitangaza Ufaransa italazimika kufunga kambi zake za kijeshi kwenye eneo lake, ilithibitisha kuwa hatua hiyo itakamilika mwishoni mwa 2025. Ivory Coast ina kikosi kikubwa zaidi kilichosalia cha wanajeshi wa Ufaransa katika Afrika Magharibi. Kuna wanajeshi 600 wa Ufaransa nchini humo na 350 nchini Senegal. "Tumeamua kwa njia ya pamoja kuondoa vikosi vya Ufaransa kutoka Ivory Coast," Rais Ouattara alisema. Aliongeza kuwa kikosi cha wa...